Mhubiri Mlango 7 Ecclesiastes

Mhubiri 7:1 Ecclesiastes 7:1

Heri sifa njema kuliko marhamu nzuri; Na siku ya kufa kuliko siku ya kuzaliwa.

Mhubiri 7:2 Ecclesiastes 7:2

Heri kuiendea nyumba ya matanga, Kuliko kuiendea nyumba ya karamu. Kwa maana huo ndio mwisho wa wanadamu wote, naye aliye hai atautia moyoni mwake.

Mhubiri 7:3 Ecclesiastes 7:3

Huzuni ni afadhali kuliko kicheko, Maana simanzi ya uso ni faida ya moyo.

Mhubiri 7:4 Ecclesiastes 7:4

Moyo wake mwenye hekima umo nyumbani mwa matanga, bali moyo wake mpumbavu umo nyumbani mwa furaha.

Mhubiri 7:5 Ecclesiastes 7:5

Heri kusikia laumu ya wenye hekima, Kuliko mtu kusikia wimbo wa wapumbavu;

Mhubiri 7:6 Ecclesiastes 7:6

Maana kama mlio wa miiba chini ya sufuria, Ndivyo kilivyo kicheko cha mpumbavu. Hayo nayo ni ubatili.

Mhubiri 7:7 Ecclesiastes 7:7

Kweli jeuri humpumbaza mwenye hekima, Na rushwa huuharibu ufahamu.

Mhubiri 7:8 Ecclesiastes 7:8

Heri mwisho wa neno kuliko mwanzo wake, Na mvumilivu rohoni kuliko mwenye roho ya kiburi.

Mhubiri 7:9 Ecclesiastes 7:9

Usifanye haraka kukasirika rohoni mwako, Maana hasira hukaa kifuani mwa wapumbavu.

Mhubiri 7:10 Ecclesiastes 7:10

Usiseme, Kwani siku za kale kupita siku hizi? Maana si kwa hekima uulizavyo neno hilo.

Mhubiri 7:11 Ecclesiastes 7:11

Hekima ni njema, mfano wa urithi; Naam, nayo ni bora kwao walionao jua.

Mhubiri 7:12 Ecclesiastes 7:12

Kwa maana hekima ni ulinzi, kama vile fedha ilivyo ulinzi; na ubora wa maarifa ni ya kwamba hekima humhifadhi yeye aliye nayo.

Mhubiri 7:13 Ecclesiastes 7:13

Tafakari vema kazi yake Mungu; kwa sababu ni nani awezaye kukinyosha kitu kile alichokipotosha yeye?

Mhubiri 7:14 Ecclesiastes 7:14

Siku ya kufanikiwa ufurahi, Na siku ya mabaya ufikiri. Mungu ameifanya hiyo moja kwenda sambamba na hiyo ya pili, ili mwanadamu asipate kulijua neno lo lote litakalofuata baada yake.

Mhubiri 7:15 Ecclesiastes 7:15

Mambo hayo yote nimeyaona mimi katika siku za ubatili wangu, yuko mwenye haki apoteaye katika haki yake, yuko na mtu mwovu azidishaye maisha yake katika udhalimu wake.

Mhubiri 7:16 Ecclesiastes 7:16

Usiwe na haki kupita kiasi; Wala usijiongezee hekima mno; Kwani kujiangamiza mwenyewe?

Mhubiri 7:17 Ecclesiastes 7:17

Usiwe mwovu kupita kiasi; Wala usiwe mpumbavu; Kwani ufe kabla ya wakati wako?

Mhubiri 7:18 Ecclesiastes 7:18

Ni vizuri kwamba ulishike neno hilo; naam, hata kwa neno hilo tena usiuondoe mkono wako; kwa kuwa mtu yule amchaye Mungu atatoka katika hayo yote.

Mhubiri 7:19 Ecclesiastes 7:19

Hekima ni nguvu zake mwenye hekima, Zaidi ya wakuu kumi waliomo mjini.

Mhubiri 7:20 Ecclesiastes 7:20

Bila shaka hakuna mwanadamu mwenye haki hapa duniani, ambaye afanya mema, asifanye dhambi.

Mhubiri 7:21 Ecclesiastes 7:21

Tena, usitie moyoni mwako maneno yote yaliyosemwa; usije ukamsikia mtumwa wako mwenyewe ali anakutukana.

Mhubiri 7:22 Ecclesiastes 7:22

Kwa kuwa mara nyingi moyo wako pia unajua ya kwamba wewe mwenyewe umewatukana watu wengine.

Mhubiri 7:23 Ecclesiastes 7:23

Mambo hayo yote mimi nimeyahakikisha katika hekima. Nilisema, Mimi nitakuwa na hekima, lakini imefarakana nami.

Mhubiri 7:24 Ecclesiastes 7:24

Mambo yale yaliyo mbali, na yale yaendayo chini sana, ni mtu yupi awezaye kuyatafuta?

Mhubiri 7:25 Ecclesiastes 7:25

Nikageuka, na moyo wangu ulikazwa katika kujua na kupeleleza, na kuitafuta hekima, na maana ya mambo yaliyoko; ili nifahamu ya kuwa uovu ni upumbavu, na upumbavu ni wazimu.

Mhubiri 7:26 Ecclesiastes 7:26

Nami nimeona lililo na uchungu kupita mauti; yaani, mwanamke ambaye moyo wake ni mitego na tanzi, na mikono yake ni kama vifungo; yeye ampendezaye Mungu atamponyoka, bali mwenye dhambi atanaswa na yeye.

Mhubiri 7:27 Ecclesiastes 7:27

Tazama, asema Mhubiri, mimi nimeyaona hayo kwa kulinganisha hili na hili, ili kuitafuta jumla;

Mhubiri 7:28 Ecclesiastes 7:28

ambayo bado nafsi yangu nikali nikiitafuta, nisiione; mwanamume mmoja katika elfu nimemwona; bali mwanamke mmoja miongoni mwa wote mimi sikumwona.

Mhubiri 7:29 Ecclesiastes 7:29

Tazama, hili tu nimeliona; Mungu amemfanya mwanadamu mnyofu, lakini wamebuni mavumbuzi mengi.